by Said A Mohamed
Mikondo mitatu ya nguvu zinavutana katika riwaya hii. Wahusika wakuu niMwenye Meno, Halima na Muuza Madafu. Mwenye Meno yumo kundini ndani na ‘wanaofanya-wafanyavyo’. huru kabisa! Wale wanaoshika sheria mikononi mwao. Wakwasi wa ajabu. Wakwasi wenye hamu isiyo na mwisho. Wenye kutaka wakapewa. Wenye kutoa kwa mtitiriko – kiasi tu mambo yawaendee kwa mapana na marefu. Hao ndio wanaokunywa sharbati, mvinyo, vinywaji baridi na vikali. Burudani yao imo ndani na nje. Hao ndio wanaocheza na maisha ya wananchi — au walalahoi! Kwa nini lakini? … Riwaya itakwambia.
Nguvu nyingine zimo ndani ya akili na ushujaa wa Halima. Yeye ni miongoni mwa wanawake wenye mwamko mkali – ambao siku hizi wanavinjari. Ni mwandishi wa habari mashuhuri anayekubalika nchini na duniani. Pia ni mwanaharakati anayechimba mashimo ya waovu chini ya ardhi au baharini. Haogopi wala hatetereki Halima. Kiasi cha kwamba humtafuta mhalifu kama juju wa majuju. Lakini Mwenye Meno naye anamtafuta Halima kwa uvumba na udi. Yuko tayari kumnunulia dunia kama si ulimwengu. Je, Halima atakubali kuogelea bahari la Mwenye Meno? … Msomaji ngojea hatima ya Mwenye Meno.
Naye Muuza Madafu ana bahati; ni sawa na mtu kuokota panga kibandani. Halima wa lulu na dhahabu, anampenda Muuza Madafu na anatosheka naye, hasa kwa ukakamavu. Watu humkejeli Halima, lakini anajua anachokifanya na anachokitaka. Je, Muuza Madafu kwa ushujaa wake ataweza kuubadili ulimwengu wa Halima kuwa wa chanda na pete kwa wawili hao? … Msomaji hudhuria arusi yao.
Reviews
There are no reviews yet.